Kapombe apelekwa Sauzi kwa matibabu


HALI ya kiafya ya beki wa Azam FC, Shomary Kapombe siyo nzuri na jana alilazimika kupelekwa Afrika Kusini kwa matibabu zaidi.

Ofisa Habari wa Azam, Jaffer Idd alisema wamelazimika kumpeleka nje ya nchi mchezaji huyo ili kupata matibabu zaidi kutokana na afya yake kushindwa kuimarika tangu alipoanza kuumwa wiki iliyopita.

Idd alisema wanaamini baada ya kufanya vipimo na matibabu huko Afrika Kusini, Kapombe atarejea katika afya yake na kuanza kuitumikia timu yake.

“Ni kweli Kapombe ameondoka nchini leo (jana) asubuhi kwenda Johannesburg kwa ajili ya uchunguzi zaidi," alisema Idd.
Aliongeza: "Alikuwa na dalili za homa ya malaria, lakini kadri muda ulivyokuwa ukienda hakuonekana kupata nafuu ya kuridhisha.”

Akiwa Afrika Kusini, Kapombe ambaye ataikosa mechi ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Esperance ya Tunisia, atafanyiwa uchunguzi wa kina kuhusu afya yake.

Kapombe pia hakuichezea mechi mbili za viporo za Azam, dhidi ya Toto Africans (1-1) Mwanza na Ndanda FC (2-2) Chamazi.

Wakati huohuo, Idd alisema kuwa Esperance wanatarajia kuwasili leo saa 4:30 usiku kwa ndege ya kukodi wakati marefa kutoka Afrika Kusini watawasili saa 12:00 jioni.

Source: ippmedia.com

About Admin

0 comments:

Post a Comment