KILIMO BORA CHA NYANYA


KILIMO BORA CHA NYANYA

NYANYA (TOMATOES)-Lycoperscon esculentum



UTANGULIZI
Nyanya ni aina ya mboga inayo zalishwa kwa wingi sana
duniani. Kwa Tanzania, nyanya ni zao la kwanza katika mazao
ya mboga linalo limwa na kuliwa kwa wingi ukilinganisha na
mboga zingine. Nyanya hutumika karibu katika kila mlo.
Nyanya ni zao umuhimu kama chakula na pia kama
zao linalomwingizia kipato mkulima.

HALI YA HEWA INAYOFAA KWA KILIMO CHA NYANYA
Mahitaji ya zao la nyanya
Nyanya hustawi vizuri kwenye maeneo ya joto, yasiyo na
ukungu mwingi hasa wakati zao linatoa maua na matunda. Zao
hili hupenda kipindi kirefu cha jua na joto ili kuongeza ukuaji wa
matunda na kupunguza magonjwa ya aina ya ukungu/kuvu. Zao
hili halipendi mvua nyingi ingawa linahitaji maji kwa wingi.
Katika kipindi chenye mvua nyingi na jua kidogo nyanya
hushindwa kutoa maua na matunda ya kutosha bali huweka
majani mengi. Katika kipindi hiki pia, nyanya hushambuliwa
sana na magonjwa ya ukungu.

UDONGO UNAOFAA KWA KILIMO CHA NYANYA
Nyanya hupendelea udongo unaopitisha maji kwa urahisi na
wenye rutuba ya kutosha na hivyo hupenda samadi. Udongo
uwe umetifuliwa vya kutosha kuruhusu mizizi kushika vema.

AINA ZA NYANYA
Kuna aina kuu mbili za nyanya kulingana na ukuaji wa mmea:
yaani:
1>> Nyanya zinzorefuka zenye kuhitaji egemezi (mfano
Money maker)

2>> Nyanya fupi zenye kutoa matawi
mengi mfano Roma,Tanya na Cal J.


KIASI CHA MBEGU
kwa ekari moja utahitaji Mbegu gram 100-150 kwa OPV variety, na Gram 30-50 kwa hybrid (F1) . Gharama za kutosha eka moja kwa OPV variety ni tsh 100,000-180,000, na kwa Hybrid (F1) Gharama ni kati ya tsh 200,000-400,000 kutegemea na aina yenyewe ya mbegu.

UKUZAJI WA MICHE YA NYANYA
Miche ya nyanya huzalishwa kwenye kitalu kwa kupanda
mbegu. Mbegu za nyanya huota baada ya siku 5 hadi 10.
Baada ya kukua kitaluni kwa muda wa wiki 4 hadi 5 toka kuota
kwa mbegu, miche hupandwa shambani. Kabla ya kupandikiza
shambani miche huandaliwa kwa kupunguza umwagiliaji maji
kwa siku moja au mbili ili miche izoee hali ngumu kabla ya
kuhamishiwa shambani.
Hapo shambani miche hupandikizwa kwa kuzamishwa katika
kina kirefu zaidi ya ilivyo kuwa kitaluni. Hii inasaidia miche kutoa
mizizi ya pembeni mingi zaidi kwa ajili ya kufyonza maji pamoja
na virutubisho aridhini. Baada ya kupandikiza mwagilia maji ya
kutosha. Usimwagilie maji juu ya mche wa nyanya. Katika
kipindi cha jua kali, tandaza nyasi kwenye tuta ili kupunguza
upotevu wa maji na unaweza kuweka kivuli kwa kutumia majani
ya miti au migomba.
Kulingana na aina ya nyanya na rutuba ya udongo, nafasi ya
kupandia ni sm 60 kati ya mstari hadi mstari na 45 hadi 60
nafasi ya mche hadi mche AU sm 90 kwa 50 AU 75 Kwa 40. Kama udongo hauna rutuba ya
kutosha inapendekezwa kutumia nafasi kubwa ya kupanda.
Utunzaji wa zao la nyanya
Nyanya fupi zisizo refuka kwenda juu, ni rahisi sana kutunza na
hazihitaji huduma nyingi. Tatizo kubwa ni kuwa kwa kutambaa
chini, katika kipindi cha mvua huwa karibu na magonjwa
yatokanayo na udongo. Katika kipindi cha jua kali, matunda
huungua kwani mmea huwa na majani machache tu yanayo
kinga matunda yasipigwe na mionzi ya jua.

MBOLEA
Licha ya mbolea ya kupandia, unashauriwa kuongeza mbolea
kipindi cha wiki mbili au tatu baada ya kupandikiza miche
bustanini. Mbolea hii ya kukuzia iwekwe kuzunguka shina la
mmea kwa umbali wa sentimeta 5 hadi saba kutoka kwenye
shina. Kwa mbolea kama vile CAN, NPK, au SA tumia kifuniko
kimoja cha soda kwa shina. Mbolea hii inaweza kuwekwa mara
mbili kabla ya mvuno wa kwanza.
Ili kurefusha kupindi cha uzaaji wa zao la nyanya (na hata
mazao mengine yatoayo matunda kama vile nyanya chungu,
biringanya, pilipili hoho, nk) inapaswa kuongezea mbolea katika
kipindi cha uvunaji mfano baada ya kuvuna mara mbili
unashauriwa kuongeza mbolea ya samadi na mbolea kama vile
NPK. Hii inasaidia mmea kuendelea kutoa maua bila kuchoka.
Kwa kawaida nyanya fupi jamii ya “Roma” huweza kuzaa na
kuvunwa kwa kipindi cha wiki 6 hadi 8 tu. Lakini kama utakuwa
unaongezea mbolea na kukazania matunzo ya bustani (hasa
usafi wa bustani na kumwagilia maji ya kutosha), nyanya
zinaweza kuendelea kuzaa kwa muda mrefu zaidi. Hii ni tofauti
na mazoea ya wakulima wengi kuwa mara nyanya zianzapo
kuzaa huduma za palizi na usafi wa shamba huachwa na kutilia
maanani kazi ya kuvuna pekee. Hii inajitokeza zaidi kwenye
aina ya nyanya fupi.
Kwa nyanya fupi ni vizuri kuhakikisha kuna matawi mengi
iwezekanavyo ili kuweza kupata matunda mengi zaidi. Hivyo
usipunguze matawi katika aina hii ya nyanya.
Kwa nyanya ndefu zenye kuhitaji egemezi,tunashauriwa kukuza
nyanya kwa tawi moja lisilo na vichipukizi pembeni au matawi
mawili na kuacha mnyanya urefuke.
Kupunguza majani ni muhimu pia katika kupunguza
maambukizo ya ukungu katika shina na pia kutoa nafasi ili
mwanga kupenya na kuruhusu mzunguko wa hewa. Majani
yapunguzwe kipindi cha asubuhi kwa kutumia mkono na siyo
kisu kwani kinaweza kueneza magonjwa kutoka mche hadi
mche.
Kwa nyanya ndefu, majani ya chini ya matunda huondolewa
kadiri unavyo endelea kuvuna. Unashauriwa upunguze majani
wakati wa asubuhi kwa kutumia mkono na pia usitoe zaidi ya
majani matatu katika mmea kwa mara moja.

UMWAGILIAJI WA NYANYA
Nyanya ni zao linalohitaji maji mengi sana kwa ajili ya ukuaji wa
mmea na matunda yake. Umwagiliaji uwe wa kulingana kwa
kila siku iliyo pangwa. Usibadilishe ovyo kiasi cha maji na ratiba
ya kumwagilia. Hii inasababisha kuoza kwa kitako cha nyanya.
Pia ili kutunza maji katika udongo, inashauriwa kuweka
matandazo katika mzunguko wa shina la nyanya au bustani
yote. Nyanya inayo kua vizuri hutumia maji lita mbili kwa siku
katika kipindi cha jua kali. Hivyo katika umwagiliaji ni busara
kuzingatia kiasi hiki cha maji katika kipindi kama hiki. Pia kama
unatumia keni, mpira au bomba usimwagilie maji juu ya matawi
ya nyanya kwani umwagiliaji wa namna hii utasababisha
kuenea kwa magonjwa ya ukungu.

CHANGAMOTO ZA KILIMO CHA NYANYA
Matatizo yanayosumbua kilimo cha zao hili ni magonjwa na
wadudu waharibifu. Hapa tutajifunza mbinu mbali mbali za
kuzuia magonjwa na wadudu waharibifu.

WADUDU WAHARIBIFU WA NYANYA
i>Funza washambuliao matunda
(Funza wa vitumba)

Huyu funza hushambulia mazao mengine kama vile pamba,
mahindi, mtama, maharage n.k. Mdudu huyu hushambulia
matunda ya nyanya kwa kutoboa na hivyo kuyafanya yapoteze
soko kwasababu hayafai kuuzwa katika soko na pia yanaweza
kuoza wakati wa usafirishaji.
Ili kuthibiti piga dawa ya kuua wadudu kama vile thiodan, sevin
ya unga, karate, selecron, n.k. Muarobaini hutumika pia katika
kupunguza uharibifu wa mdudu huyu.

ii>Inzi weupe
Wadudu hawa huruka ruka kwenye shamba la nyanya na kukaa
chini ya majani. Mdudu huyu hueneza magonjwa ya virusi kama
vile “ukoma wa nyanya”. Usafi wa shamba na mazingira ya yake ni
muhimu katika kupunguza kuzaana kwa wadudu hawa.

Ili kuthibiti wadudu hawa kwenye bustani ya mboga na pia
katika maficho yao, piga dawa kama vile karate,
cypermethrin mara kwa mara.

Panda mimea mingine (kama vile tumbaku) inayo vutia
wadudu hawa kwenye maeneo ya bustani kisha piga dawa
katika miche ya tumbaku ili kuwaangamiza kwa wingi.

iii>Minyoo
Mdudu huyu hukaa kwenye udongo wenye
unyevu wa kutosha. Huvamia mizizi ya nyanya na
kuharibu mfumo wa usafirishaji maji na chakula
kwenye nyanya iliyo athirika. Uking'oa mche wa
nyanya utaona vifundo kwenye mizizi.
Kuzuia
Mbinu za kuthibiti ongezeko la wadudu hawa ni kuharibu hali ya
udongo inayo mfanya aishi na kuzaana. Mbinu hizi ni:

Kulima shamba kwa kutifua baada ya kuvuna nyanya ili
udongo wa chini ukae juani na kukauka. Hii inasaidia
kuangamiza wadudu hawa kwa joto na ukosefu wa maji.

Choma moto na kuteketeza mabaki ya nyanya baada ya
kuvuna.

kuzungusha aina ya zao la nyanya au jamii ya nyanya na
mazao mengine yasiyo vamiwa na adui huyu. Hii
huwafanya minyoo wasipate hifadhi na chakula kutoka
kwenye mimea wanayo tumia kuishi na kuzaliana. Hivyo
idadi yao kupungua katika udongo.

kabla ya kupanda zao weka samadi nyingi katika udongo
kwenye eneo lililo athiriwa na wadudu hawa kwani
hawapendi udongo wenye samadi nyingi.

Panda manung'a nung'a (
Tagetes spp
) katika eneo
lililoathirika na minyoo hawa, mimea hii hutoa sumu ya
aina fulani ambayo huathiri ukuaji na kuzaliana kwa
minyoo hawa.

MAGONJWA YA NYANYA
Uchunguzi umeonyesha kuwa nyanya na mazao mengine jamii ya nyanya ndiyo
hushambuliwa sana na magonjwa kuliko mazao mengine ya
mboga.

i>UKUNGU
Huu ni ugonjwa unaopenda hali ya unyevu mwingi hewani.
Hivyo hujitokeza zaidi wakati wa masika. Pia sehemu zenye
umande mwingi wakati wa usiku, ugonjwa huu hujitokeza hata
wakati wa kiangazi
Dalili za ukungu katika nyanya
Ugonjwa huu hushambulia shina, maua na matunda. Kuungua
kwa majani kama vile yamechomwa na maji moto. Chini ya jani
utaona unga unga mweupe. Matunda pia hushambuliwa na
ugonjwa huu na hugeuka kuwa meusi na magumu.
Kuzuia

Inabidi kuchanganya mbinu mbali mbali za kupambana
na ugonjwa huu.

Kwanza ni usafi wa shamba kwa ujumla yaani
hakikisha unaondoa magugu katika bustani.

Tandaza nyasi juu ya matuta yaliyo pandwa nyanya.

Ondoa majani yaliyo zeeka na yanayo onyesha dalili za
ugonjwa huu. katika kupunguza majani, hakikisha
sehemu za chini ya mmea ni wazi na kuna mzunguko
mzuri wa hewa. Punguza majani katika mmea ili
kupunguza umande na ukungu kwenye mmea.

Baada ya kupunguza majani na machipukizi hakikisha
unatupa mbali majani hayo na siyo kuyaacha kwenye
tuta la bustani.

Ondoa kabisa mmea ulio na dalili za ugonjwa huu

Kupiga dawa katika kipindi cha mvua mara baada ya
mvua kubwa. Fanya hivyo mara moja au mara mbili
kwa wiki kutegemea na wingi au mfululizo wa mvua.
Unapoona jua limetoka piga dawa ili ugonjwa
usijitokeze tena.
Baadhi ya madawa yanayofaa kukinga ugonjwa huu ni Dithane
M45, Bravo, Benlate , Ridomil, Topsin n.k. Kumbuka kuwa kila
mwaka madawa yenye nguvu zaidi hutengenezwa, hivyo uliza
watalaam walioko karibu nawe. Ingawa Blue Copper inauzwa
kwa bei nafuu, nguvu yake in kidogo sana kuthibiti huu
ugonjwa.
Muarobaini pia unaweza kutumika kupunguza ugonjwa huu.
Changanya unga unaotokana na mbegu za muarobaini kiasi
cha nusu kilo ya unga katika lita 20 za maji.

ii>Ugonjwa wa ukoma wa nyanya
Huu ni ugonjwa wa virus unao enezwa na inzi mweupe. Inzi
hawa hushambulia zaidi nyanya wakati wa kiangazi, hasa
kipindi cha joto kali.
Dalili

Majani machanga hujikunja na baadaye majani yote.

Kupungua kwa utoaji maua na matunda na hata
yakitokea matunda huwa ni madogo.

Mmea kudumaa na kutozaa kabisa.
Kuzuia
Mbinu madhubuti ni kupunguza kuenea kwa ugonjwa huu
kwenye shamba kwa kudhibiti kuzaana na kuenea kwa mdudu
(inzi mweupe) kama tulivyo ona katika kupambana na mdudu
huyo, yaani:

Kuondoa mimea michache iliyo shikwa na ugonjwa
maana wadudu hawa wanachukua ugonjwa huu kutoka
mimea hii.

Kutumia mbegu zilizo hakikishwa kuwa zinaweza
kuvumilia ugonjwa huu na kutoa mavuno mazuri.

Usilime nyanya karibu na eneo lililo na mazao kama
bamia,mipapai maana mimea hii huhifadhi inzi
mweupe.

Kuua inzi weupe wanaofyonza nyanya na kusambaza
virusi kwa kutumia madawa. Tumia madawa kama vile
Selecron, Decis, Karate n.k.

Epuka kuchanganya zao la nyanya na mazao mengine
yanayohifadhi hawa nzi kama vile mipapai na bamia.

Ng'oa na kuchoma moto mimea yote iliyougua ugonjwa
huu.

iii>Ugonjwa wa mmea wa nyanya kuoza sehemu ya shina
inayogusa udongo na mmea kunyauka kama vile umekosa
maji

Wadudu wanaosabisha ugonjwa huu hupatikana ardhini.

Hakuna dawa ya kutibu ugonjwa huu baada ya dalili
kujitokeza.

Kupiga madawa za viwandani ardhini kabla ya kupanda
nyanya husaidia kupungu wadudu wa ugonjwa.

Epuka kupanda nyanya au mazao jamii ya nyanya katika
eneo moja kwa muda mrefu mfulilizo . Baadhi ya mazao
yanayohusiana na nyanya ni bilinganya, pilipili, ngogwe,
mnavu, n.k.

iv>Ugonjwa wa miche michanga ya nyanya kuoza sehemu ya
shina inayogusa udongo na kufa ghafla
Ugonjwa huu hushambulia miche kitaluni na husabishwa na
wadudu waishio ardhini. Mara baada ya dalili, ugonjwa huu
hauna dawa ila unaweza kukingwa kwa kutumia njia zifuatazo:

Choma moto udongo wa kutengezea kitalu kabla ya
kupanda mbegu zako. Kutumia mboji husaidia kukinga
miche dhidi ya ugonjwa huu.

Epuka kumwagilia maji kupita kiasi na kutumia kuvuli
kizito.

v>Matunda ya nyanya kuoza kitako.
Huu ni ugonjwa unaosababishwa na:

Umwagiliaji wa nyanya bustanini usio na mpangilio
maalumu. Mfano, kumwagilia mimea maji mengi kisha
kuiacha bila maji kwa siku kadhaa.


vi>Upungufu wa virutubisho aina ya chokaa.
Dalili zake ni matunda ya nyanya kuoza sehemu ya kitako na
kuonyesha rangi nyeusi.
Kuzuia ugonjwa huu, zingatia kuwa na utaratibu mzuri wa
kumwagilia maji ambao haubadiliki ovyo kiratiba na kiasi cha maji
yanayowekwa. Rutubisha mimea kwa madini ya chokaa kwa
kutumia mbolea aina ya CAN zenye madini haya.

UVUNAJI WA NYANYA
Nyanya za kupelekwa sokoni zinabidi ziwahi kuvunwa mara tuuzinapoanza kuiva ili kuzifanya ziwe salama kipindi cha kusubiri kuuzwa na kusafirishwa.
Nyanya zinazopelekwa viwandani zinatakiwa zivunwe baada ya kukamilika uivaji wake.Ili kuzisafirisha nyanya vizuri tumia maboksi ya mbao.

About Admin

0 comments:

Post a Comment