KILIMO BORA CHA VITUNGUU

KILIMO BORA CHA VITUNGUU

KITUNGUU-ONION (Allium cepa)



UTANGULIZI

Vitunguu ni zao la pili ambalo hutumika karibu kila siku katika mlo
wa familia za kitanzania. Vitunguu vina chukua nafasi kubwa katika
matumizi ya mboga hasa kwa wakazi wa mijini. Vitunguu hutumika
katika kutengeneza kachumbari, kiungo cha mboga, nyama na
samaki. Majani ya kitunguu hutumika kama mboga. Vitunguu pia
hutumika kutengeneza supu. Vitunguu huweza kutoa Tani 10 hadi 16 Kwa ekari (magunia 80 hadi 160).

HALI YA HEWA NA UDONGO UFAAO KWA KILIMO CHA VITUNGUU
Zao la vitunguu hustawi vizuri kwenye maeneo yasiyo na mvua
nyingi sana, yenye baridi kiasi wakati wa kiangazi na yasiyo na joto
kali pamoja na ufukuto wa ukungu wakati wa kukomaa vitunguu.
Zao la vitunguu hustawi vizuri kwenye udongo wenye rutuba ya
kutosha. Udongo unao ruhusu mizizi kupenya kirahisi, unao hifadhi
unyevu kama vile udongo wa mfinyanzi tifutifu.
Upandaji wa mbegu za vitunguu
Hapa Tanzania upandaji wa mbegu za vitunguu katika kitalu kwa
ujumla huanza mwezi machi hadi mei kutegemea na msimu wa
kilimo. Hivyo kilimo hiki hufanyika mara baada ya mvua za masika
kubwa kuisha. Kipindi cha kiangazi na baridi huruhusu ukuaji mzuri
wa vitunguu. Kiasi cha Kilogram 1.5 hadi 2 za Mbegu Hutosha kwa ekari moja.
Mbegu za vitunguu huoteshwa mapema katika kitalu. Mbegu
zinaweza kupandwa kwa mstari au kwa kutawanya katika tuta la
kitalu. Katika upandaji wa mstari, mbegu hupandwa katika nafasi
ya sm 10 hadi 15 kati ya mstari na mstari.
Baada ya kupanda, mbegu hufunikwa kwa udongo na baadaye
kwa kuweka matandazo juu ya tuta. Mara baada ya mbegu kuota,
matandazo yaondolewe na badala yake kichanja cha nyasi
kijengwe ili kuiwekea kivuli mimea michanga. Mbegu huota baada
ya siku 7 hadi 10.www.kilimofaida.blogspot.com

KUPANDIKIZA MICHE YA VITUNGUU BUSTANINI
Upandikizaji wa miche ya vitunguu bustanini hufanyika baada ya
miche kukua na kufikia ukubwa wa unene wa penseli. Mara nyingi
miche hii itakuwa imesha kaa kitaluni kwa siku 40 baada ya mbegu
kupandwa.
Usichelewe kuhamisha na kupandikiza miche hii bustanini. Kwa
sababu miche mikubwa sana itaweza kutoa maua badala ya kutoa
tunguu. Na hivyo mara nyingi vitunguu namna hii hubaki na suke la
maua.
Wakati wa kupandikiza miche haishauriwi kukata wala kupunguza
majani. Miche ipandikizwe katika nafasi ya sm 30 kati ya mstari na
mstari na sm 10 kati ya mche na mche.


Upandaji wa miche bustanini unaweza kufanyika kwenye mistari
katika matuta au kwenye vijaruba. Vijaruba vya mraba hutumika
kwenye maeneo yenye ardhi tambarare na iliyo kame ili kuhifadhi
maji baada ya kumwagilia. Kwa sehemu zenye udongo mzito na
zenye maji mengi tumia matuta yenye mwinuko wa sm 10 hadi sm
15 kutoka usawa wa ardhi.
Matunzo ya bustani ya vitungu.

UMWAGILIAJI
www.kilimofaida.blogspot.com
Zao la vitunguu linahitaji maji ya kutosha katika kipindi chote cha
ukuaji wa mmea na hasa wakati wa kutunga tunguu.
Katika kipindi kisicho na mvua (mwezi mei hadi Agosti) umwagiliaji
ufanyike mara moja kwa wiki kwa udongo wa mfinyanzi tifutifu na
vitunguu vilivyopandwa katika vijaruba.
Ili kuharakisha kukomaa kwa vitunguu unashauriwa kupunguza
kiasi cha maji ya kumwagilia taratibu kadri zao linavyo kua. Pia ni
vizuri uache kumwagilia maji mapema wiki nne hadi sita kabla ya
kuvuna. Kwani muda kamili wa kukomaa na kuvuna kwa vitunguu
ni siku 90 hadi 150 kutegemea na aina ya mbegu.
Kuthibiti magugu na kupandishia udongo
Kitunguu ni zao lisilo weza kushindana na magugu. Magugu
husababisha kupungua kwa ukubwa wa kitunguu, hueneza
magonjwa na husababisha kudumaa kwa vitunguu.
Katika bustani ya vitunguu, magugu yanaweza kutolewa kwa njia
ya kutifulia kwa jembe dogo, kung'olea kwa mkono na pia kwa
kutumia madawa ya kuua magugu.
Kama unaondoa magugu kwa kutifulia, epuka kutifua kwa kina
kirefu ili kutoharibu mizizi na vitunguu vyenyewe, kwani mizizi ya
vitunguu ipo juu juu sana.
Kupandishia udongo kwenye mashina ya vitunguu ni hatua
muhimu ili vitunguu visiunguzwe na jua. Hakikisha kuwa
mashina ya vitunguu vyako ndani ya udongo kama
sentimita 5. Pia kuna aina ya vitunguu ambavyo hutoa au
hupandisha tunguu lake juu ya udongo wakati vinapokua.
Hivyo kupandishia udongo ili kufunika tunguu ni muhimu
sana.


MAGONJWA YA VITUNGUU NA WADUDU WAHARIBIFU

WADUDU WAHARIBIFU

Kuna aina tatu za wadudu wanao haribu zao hili:

1>Viroboto wa vitunguu
Hawa ni wadudu waharibifu namba moja wa zao la vitunguu hapa
nchini Tanzania. Husababisha upotevu mkubwa wa mavuno.
Wadudu hawa huonekana hasa wakati wa kipindi cha joto.
Dalili za kugundua
Majani yaliyo shambuliwa na wadudu hawa huwa na mabaka
meupe yenye kung'aa. Katika hali iliyo kithiri majani yote hugeuka
kuwa na tabaka nyeupe au kijivu cheupe na baadaye majani
hunyauka kabisa.
Kuzuia

Mdudu huyu huzuiwa kwa kupiga dawa kama vile thiodan-35,
Parathion nk.

Ili kupunguza uvamizi mkubwa, panga upandaji wa vitunguu
mapema ili kipindi cha joto kiingiapo zao lako liwe limekomaa.

Epuka kupanda zao la vitunguu sehemu iliyo kuwa na mazao
aina ya vitunguu kama vile liksi, vitunguu swaumu, n.k.

2> funza na minyoo ya mizizi
wanakata miche .

Hawa hupigwa vita kwa kuzingatia mzunguko wa mazao
bustanini.

MAGONJWA YA VITUNGUU

a) Ukungu mweupe
Ugonjwa huu hujionyesha kipindi cha baridi iliyo ambatana na
unyevunyevu mwingi hewani.
Dalili za kugundua Ugonjwa huu

Utaona unga unga wa rangi ya zambarau katika majani.

Majani hugeuka rangi na kuwa njano na baadaye
kunyauka.

Ugonjwa huu hupenya hadi chini kwenye tunguu na
kusababisha kuoza kwake.
Kuzuia

Unashauriwa kubadili aina ya zao katika shamba lako
kwa kupanda mazao mengine yasiyo jamii ya vitunguu.
Kilimo cha mzunguko wa aina mbalimbali za mazao
upangwe kiasi kwamba vitunguu visipandwe eneo moja
mpaka baada ya miaka 3 kama ugonjwa ulikuwa
mwingi.

Tumia dawa za kuzuia ukungu. Hii ifanyike kabla ya
kuona dalili za ugonjwa kwenye vitunguu. Piga dawa
kama vile maneb, dithane M45, zineb ya unga, n.k.
Wakati unapoona hali ya hewa inayo wezesha kuenea
kwa ugonjwa huu (yaani baridi iliyo ambatana na
unyevunyevu mara kwa mara). Katika kipindi hiki piga
dawa kila baada ya siku sita ili kuzuia kuingia kwa
ugonjwa. Ugonjwa ukisha ingia kwenye mimea
hauzuiliki kwani hakuna dawa ya kuponyesha.

b) Ukungu wa kahawia
Ugonjwa huu unaweza kuleta madhara makubwa wakati
vitunguu vikiwa bustanini na hata wakati vikiwa katika ghala.


Dalili zake
Vikovu vya mbonyeo hujitokeza kwenye majani na baadaye
hutoa doa la rangi ya zambarau. Vikovu hivi hukua na
kutengeneza vidonda ambavyo hukua na kufanya mzunguko
katika jani zima au shina la kitunguu. Baada ya wiki kama tatu
hivi tangu kuingia kwa ugonjwa huu, majani yote huanguka na
kukauka.
Ugonjwa huu hushambulia vitunguu hata baada ya kuvuna kwa
kupitia shingo ya kitunguu au sehemu yoyote yenye kovu,
kidonda au mkwaruzo.
Namna ya kuzuia

Katika bustani, mara uonapo kitunguu chenye dalili za
ugonjwa huu, ondoa mimea na kuiteketeza kwa moto ili
kuzuia au kupunguza kuenea kwa ugonjwa.

Kwa kinga ya bustani, piga dawa za Dithane M 45 na dawa
zingine za kuzuia magonjwa ya ukungu. Dawa hizi zitasaidia
kupunguza kutawanyika kwa ugonjwa.

Tumia kilimo cha kuzungusha au kubadilisha mazao katika
eneo la bustani yako. Usipande mfululizo jamii yoyote ya
vitunguu katika shamba ulilovuna vitunguu.

Wakati wa kuvuna, epuka kukata au kusababisha vidonda
katika vitunguu, yaani vuna kwa kung’olea na siyo kwa
kuchimba na jembe.

Baada ya kuvuna anika vitunguu juani kwa siku moja au mbili
kabla ya kuviweka katika magunia au ghala.

c) Ugonjwa wa kuoza mizizi
Huu ni ugonjwa unaotoka udongoni na unasababishwa na
vimelea vya jamii ya ukungu.
Dalili
Dalili za ugonjwa huu ni mizizi kugeuka rangi na kuwa njano na
baadaye kuwa zambarau. Baada ya muda ugonjwa huenea na
mizizi hufa kwa kunyauka. Majani nayo hugeuka kuwa na rangi
ya njano na kisha shina au mche mzima hunyauka.
Kuzuia

Tumia kilimo cha kuzungusha mazao badala ya kupanda
vitunguu katika eneo moja toka msimu moja hadi
mwingine.

Panda aina za vitunguu zinazo vumilia ugonjwa huu kwa
mfano: Excel, L 36, Granex, White Granex na red creole.
Uvunaji wa vitunguu
Kwa ujumla uvunaji vitunguu hufanyika baada ya siku 90 hadi
150 tangu kupanda kwa miche yaani miezi mitatu hadi mitano
tangu miche kupandikizwa bustanini.
Utagundua kuwa vitunguu viko tayari kuvunwa baada ya kuona
kuwa karibu asilimia 50 au nusu ya mimea shambani inaanza
kuanguka na majani kukauka.
Ili kurahisisha ukaushaji na hifadhi sahihi ya vitunguu, pangilia
vizuri msimu wa kupanda ili kwamba uvunaji ukutane na kipindi
cha joto na kiangazi.
Uvunaji ufanyike kwa kung'oa baada ya kumwagilia maji bustani
siku moja kabla ya kuvuna.
Baada ya kuvuna kata majani kama sentimeta 2 juu ya tunguu.
Pia kata mizizi mirefu kwa sm 2 (usikate chini sana ya shingo
wala kitako cha kitunguu kwani hii husababisha kuoza kwenye 26
ghala au gunia la kusafirishia na kuenea kwa magonjwa. Baada
ya hapo kitunguu kianikwe juani kwa siku 1 hadi 2.
Vitunguu vilivyo anikwa vizuri ni vigumu kwa kubonyeza kwa
kidole gumba pia shingo ya kitunguu huwa kavu.
Mavuno ya vitunguu vilivyo tunzwa vizuri yaweza kufikia tani 7
hadi 10 kwa hecta.
Baada ya kuvuna na kuanika:

Chagua vitunguu vizuri, tenga vibovu na vilivyo vidogo
sana

Ondoa vitunguu vilivyo na makovu pamoja na vile vyenye
shingo nene (shingo ya chupa).

Undoa maganda yanayo pepea ovyo.
Baada ya uchambuzi huu, hifadhi vitunguu kwenye ghala kama
husafirishi na kama unasafirisha pakia vitunguu katika magunia
yenye kupitisha hewa ya kutosha.
Katika ujazaji wa magunia usishindilie na wala usiweke
vitunguu vichache katika gunia. Kushindilia sana vitunguu
hubabisha mkandamizo mkubwa na hivyo kuoza kwa vitunguu,
na usipojaza vizuri vitunguu katika magunia hutokea msuguano
wakati wa kusafirisha na hivyo kusababisha vidonda vitakavyo
fanya vitunguu kuoza.
Kama vitunguu havisafirishwi kwa ajili ya soko, vinaweza kutunzwa
katika sehemu kavu
iliyo na mzunguko mzuri wa hewa ya kutosha.
Vitunguu kama vile aina ya Red Creole na Texas Grano
vinahifadhika vizuri. Kwa vitunguu vilivyo hifadhiwa vizuri, huweza
kudumu hadi miezi 6 bila kuharibika. Kwa sehemu zilizo na joto
kali, usihifadhi vitunguu zaidi ya miezi mitatu kwani vitunguu
huanza kuoza na au kuchipua.
Picha ya vitunguu vya Red Creole



Picha ya vitunguu vya texas Grano

About Admin

0 comments:

Post a Comment